Sunday, June 19, 2011

HAVING THE RIGHT ATTITUDE

Abdallah ni miongoni mwa watu wenye ujasiri na uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto za maisha. Ni jasiri kwa sababu ameweza kupambana na ulemavu wa macho alioupata ukubwani, na kuhakikisha anajitafutia maisha kwa njia halali. Yeye kwa sasa ni miongoni mwa mafundi hodari wanaokubalika ndani na nje ya nchini. Je, ilikuwaje hata akawa katika hali ya ulemavu aliyonayo sasa?


Nyangalio alipohitimu shule alifanya biashara kwa lengo la kutafuta mtaji kumuwezesha kutimiza ndoto za kuondokana na umasikini, lakini aliugua na kupofuka macho hivyo kujikuta katika kundi la watu wenye ulemavu. Kupofuka kwake kulikuwa mtihani mkubwa sana, lakini hakukata tamaa ya maisha, bali alikuwa mwepesi kukubali kuishi katika hali iliyomkuta, kisha kutafuta mbinu zitakazomuwezesha kujipatia kipato ili kuepuka kuishi maisha tegemezi.

Uwezo wake wa kukabiliana na changamoto za maisha ndio uliomfanya Nyangalio kuwa fundi stadi wa nguo na habari zake zimeweza kusambaa sehemu mbalimbali Afrika Mashariki na Kati kama kielelezo kwamba ulemavu sio mwisho wa maisha. 

Mnamo mwaka 1988, Abdalah alipata maumivu makali ya kichwa yaliyoambatana na kukosa usingizi, hali hiyo ilisababisha aende katika hospitali mbalimbali kutafuta tiba bila mafanikio. Baada ya kufanyiwa uchunguzi katika hospitali ya Muhimbili, Nyangalio aliambiwa kuwa tatizo la kukosa usingizi linatokana na hitilafu iliyojitokeza katika mishipa ya macho na tiba pekee ni upasuaji utakaomfanya kuwa kipofu kwa maisha yake yote.

Abdalah anakiri kuwa ilikuwa vigumu kukubaliana na hali hiyo kwa sababu alishindwa kutambua mchana na usiku kutokana na kiza kinene kilichotanda kwenye macho yake. Alihofia kuishi maisha tegemezi. Hata hivyo daktari aliyemfanyia upasuaji alimfariji na kumpa nafasi ya kukaa katika hospitali ya Muhimbili kwa miezi mitatu akipewa ushauri pamoja na mbinu za kuishi katika hali ya kutoona. Anasema mbinu hizo alizojifunza ni pamoja na elimu juu ya maisha na changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu na jinsi ya kupambana nazo, 
Pia alifundishwa kusoma maandishi maalumu kwa watu wasioona, kutumia cherehani pia jinsi ya kukata na kushona nguo mbalimbali.

Baada ya kutoka hospitalini, alikutana na changamoto nyingi katika maisha kwa kuwa baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki walimuona kama mzigo hivyo baadhi ya ndugu walilumbana wakitupiana jukumu la kumtunza.

Anasema pamoja visa na mikasa iliyompata aliweka mikakati ya kushinda changamoto katika maisha ili aweze kuudhihirishia ulimwengu kuwa binadamu ameumbwa ili aweze kukabiliana na taabu mbalimbali kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu. Aliendelea kumuamini na kumtegemea Mungu kwa kila jambo alilolifanya huku akiwa na matumaini makubwa kuwa Mungu atampa njia nyingine ya kuishi bila ya kuwa tegemezi. 

Baada ya miezi saba ya ugonjwa alirudi katika shughuli za biashara ndogo ndogo kwa kuuza nguo za mitumba pamoja na kushona nguo kwa kutumia cherehani ya jirani yake. Alidunduliza mtaji mpaka alipopata uwezo wa kununua cherehani yake na kuanza kazi ya kushona nguo mbalimbali hasa sare za wanafunzi wa shule ya msingi. Pia alijiimarisha kiuchumi na kurudia maisha ya kujitegemea kama kiongozi wa kaya.

Kipaji cha Nyangalio alianza kufahamika mwaka 1994 wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu wa macho maarufu kama siku ya Fimbo Nyeupe Duniani. 

“Wakati wa maadhimisho hayo mgeni rasmi alisifia suti aliyokuwa amevaa aliyekuwa kiongozi wa taasisi ya wasioona. Kisha akaambiwa kuwa suti hiyo ilishonwa na fundi asiyeona hivyo nikaanza kujulikana kuanzia siku hiyo,” anasema Nyangalio anayekumbuka kuwashonea nguo Anna Abdallah, wakati huo akiwa Waziri wa Afya, Sophia Simba, Joel Bendera na wengine wengi. 

Hivi sasa Nyangalio anafanyia shughuli zake Mbagala Kibonde Maji jijini Dar es Salaam ambako amejenga makazi yake ya kudumu, amefanikiwa kusajili kampuni inayojulikana kama Nyangalio Fashion Centre ambayo ana mpango wa kuitumia kutoa elimu ya ufundi cherehani hususani kwa watu wasioona. 

Nyangalio amewahi kutoa elimu ya ushonaji kwa watu wenye ulemavu ambayo yalifadhiliwa na Taasisi ya Taifa ya Huduma ya Maendeleo ya Wasioona (TNIB), ambapo wanafunzi wanne walihitimu na kufaulu kwa kiwango cha kuridhisha.

Hivi sasa ana mashine mbili za kushonea ambazo anategemea kuzitumia kutoa mafunzo. Anaomba watu wenye uwezo kumsaidia ili kupata wafadhili wa kutimiza ndoto zake za kuanzisha shule ya ushonaji hususani kwa watu wenye ulemavu. 

Ustadi wa Nyangalio umemuwezesha kushiriki katika maonyesho mbalimbali ya ujasiriamali yaliyofanyika nchini pia katika nchi za Zambia na Kenya. Huyo ndiye Abdallah Nyangalio ambaye hakukata tamaa baada ya kupata ulemavu, bali aligeuka kuwa jasiri kiasi cha sasa kuwa mmoja wa watu wa kuiga mfano.

No comments:

Post a Comment